Mashabiki na wapenzi wa klabu ya
soka ya Jamuhuri yenye maskani yake mitaa ya Chasasa Wete Pemba wamesifu
usajili uliofanywa na Uongozi wa klabu hiyo lakini wakasema bado tatizo
linaloikabili klabu hiyo kongwe ni benchi la ufundi .
Wakizungumza na mwandishi wa
habari kwenye mazoezi ya klabu hiyo yanayoendelea katika uwanja wa Utaani
mashabiki hao wamesema kuwa usajili uliofanywa ni mzuri na unawapa matumaini ya
klabu yao kurejea ligi kuu ya Zanzibar kwa msimu ujao .
Wameutaka Uongozi wa klabu
kuhakikisha kwamba wanatafuta kocha mwenye uwezo na ambaye mbinu atakazowapa
zitakuwa ni chachu ya ushindi wa klabu kwenye michuano ya Ligi daraja la kwanza
Taifa Pemba baada ya kushuka daraja msimu uliopita .
“Usajili ni mzuri na wachezaji wote
wanaonyesha kiwango lakini bado tatizo ni kocha mwenye uwezo na sifa za
kufundisha timu , ni vyema uongozi ukatafuta kocha ambaye atakuwa ni chachu ya
ushindi wa klabu yetu ”alieleza shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Khamis .
Hata hivyo nahodha wa timu hiyo
Mfaume Shaban ameutetea uongozi wa klabu na kusema kuwa kocha aliyepo anatosha
na kuongeza kwamba wachezaji wenyewe wanatakiwa kujituma na kujitoa kwa ajili
ya timu yao wawapo uwanjani .
“Hata kama atakuja kocha Ulaya
lakini wachezaji kama hawatakuwa na moyo wa kujituma basi mafanikio
yatakuwa mbali cha msingi ni wachezaji kutambua wajibu na dhamana waliyonayo
kwa klabu na mashabiki wao ”alisisitiza Mfaume .
Mafaume amewataka mashibi na wapenzi
wa klabu hiyo kumwamini kocha aliyepo kwani anauwezo wa kuirejesha timu ligi
Kuu ya Zanzibar msimu ujao na kuwaomba wachezaji na mashabiki kuwa kitu
kimoja ikiwa ni pamoja na kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu unapokuwa
uwanjani .
Kwa upande wake Meneja wa Klabu hiyo
Mohammed Abdalla Elisha amesema kuwa kwa kipindi hichi timu itaendelea kuwa chini
ya kocha Hamad Mzee akisaidiwa na Ameir Chuwan na Juma Chande huki Ayoub Khamis
Gopi akiwa ni kocha wa makipa .
Timu ya Soka ya Jamuhuri inatarajia
kushuka kwenye kiwanja cha Polisi Finya kucheza na timu ya Algezeera katika
michuano ya ligi daraja la kwanza Taifa Pemba ikiwa imepangwa kundi moja na
klabu ya Chipukizi FC .
0 comments:
Post a Comment