Imetimia miaka mitano tangu watu 21 walipopoteza maisha yao kwenye
tamasha la muziki wa aina ya techno linalofahamika kama Loveparade na
lililofanyika mjini Duisburg nchini Ujerumani.
Kwanini? Hilo ndilo swali ambalo kila siku linavuruga mawazo ya Jörn
Teich. Kwa nini palikuwa na kibali cha kufanya tamasha hili kwenye
uwanja ambao usingetoshea idadi kubwa hivyo ya watu? Jörn Teich mwenye
miaka 41 ni muuzaji wa maua. Anahofia kwamba hatakaa apate majibu ya
maswali yake. Kila wakati Jörn anakumbuka siku hiyo ilivyokuwa, jinsi
alivyokazana kutoka nje ya uwanja wa tamasha. Amepata matatizo ya
kisaikolojia, hawezi tena kufanya kazi. "Maisha yangu yamebadilika kwa
asilimia 100. Mimi si yule niliyekuwa zamani," anasema Jörn. "Zamani
nilikuwa natoka na kustarehe. Sasa hivi sichangamani na watu, niko
kivyangu. Nimebakiwa na marafiki wachache sana. Naishi mwenyewe na binti
yangu na nimekubaliana na hali halisi."
Mara kwa mara Jörn anakwenda kwenye ngazi fulani ya kwenye uwanja wa
tamasha ilipofanyika Loveparade. Ni ngazi ambayo kwake ilikuwa ukombozi,
yeye aliweza kupanda na kutoka, wengine walifia hapo kwa kukanyagwa na
wengine.
Maisha yabadilika
Katika ngazi hiyo amekaa mtu anayejitambulisha kwa jina la
Georg. Yeye alikuwa mtaalamu wa kutoa huduma ya kwanza, alihudhuria
tamasha, si kikazi bali kwa ajili ya kuburudika na muziki. Balaa
lilipoanza kutokea, Georg aliwasaidia majeruhi. Mama mmoja alifia
mikononi mwake, juhudi zote za kumwokoa ziligonga mwamba. Hakuruhusiwa
kuendelea na kazi yake ya kutoa huduma ya kwanza. Mwajiri wake
alimwambia ni kwasababu ya athari za kisaikolojia alizopata. "Ilikuwa
ngumu sana kwangu, nilikuwa na uchungu. Katika miaka mitatu ya kwanza
nilikaribia kujiua."
Jörn Teich anasema yeye sasa amekuwa mwangalifu zaidi: "Nikifika kwenye
sherehe yoyote ile, cha kwanza ninachofanya ni kuangalia mlango wa
dharura ulipo. Nafikiria namna nitakavyoweza kutoka kwa haraka. Hicho
ndicho tunachowaza sisi tuliokuwepo siku hiyo"
Miaka mitano baada ya maafa ya tamasha la Loveparade, bado hakuna
aliyehukumiwa kwa makosa yaliyofanyika. Wahusika wanatupiana lawama.
Jörn, Georg na wenzake wanasema wameshakata tamaa na hawaamini kama ipo
siku ambayo watashuhudia mtu akipelekwa gerezani kwa damu ya watu 21
iliyomwagika miaka mitano iliyopita.
0 comments:
Post a Comment