KIKAO CHA TFF, YOUNG AFRICANS | TFF YATEUA KAMATI YA LESENI ZA KLABU | TFF YATANGAZA KOZI ZA UKOCHA |TFF YATOA KALENDA YA MWAKA, USAJILI KUANZA JUNI 15

KIKAO CHA TFF, YOUNG AFRICANS

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), leo Juni 7, 2016 limefanya kikao cha pamoja na uongozi wa Klabu ya Young Africans.

Kikao hicho kilifanyika ofisi ya TFF iliyoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Rais wa TFF Jamal Malinzi kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine; Kaimu Mkurugenzi wa Sheria na Uanachama, Elliud Mvella; Makamu Mwenyekiti wa Young Africans, Clement Sanga na Katibu Mkuu wa Young Africans, Baraka Deusdedit.

Baada ya mazungumzo, Rais wa TFF, Malinzi ametoa maelekezo yafuatayo:-
1.   Mchakato wa Uchaguzi wa Young Africans uendelee.
2.   Mchakato huo usimamiwe na Kamati ya Uchaguzi ya Young Africans chini ya uangalizi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
3.    Wale wote waliochukuliwa fomu za uchaguzi wa Young Africans katika ofisi za TFF washirikishwe kwenye mchakato huo.
Mwisho, Rais wa TFF Jamal Malinzi amewatakia kila la kheri wanachama na  wapenzi wa Young Africans na kuwa na umoja na mshikamano kuelekea uchaguzi huo muhimu wa kwa mustakabali wa klabu.

TFF YATEUA KAMATI YA LESENI ZA KLABU

Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeteua Kamati ya Leseni (Club Licensing Committee) ambayo ndiyo yenye jukumu la kupitia maombi ya leseni kwa klabu za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza na kutoa uamuzi kwa kuzingatia Kanuni ya Leseni ya Klabu.

Wajumbe walioteuliwa kwenye Kamati hiyo inayoundwa kwa mara ya kwanza ni Wakili Lloyd Nchunga (Mwenyekiti), Wakili Emmanuel Matondo (Makamu Mwenyekiti), David Kivembele, Hamisi Kissiwa na Prof. Mshindo Msolla.

Klabu zinatakiwa kuchukua fomu za maombi TFF ambapo baada ya kuzirejesha zitafanyiwa kazi ambapo zile zitakazokuwa zimekidhi matakwa ya Kanuni husika zitapatiwa leseni husika ili zishiriki michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kwa msimu wa 2016/2017.

Kwa klabu ambazo zitashindwa kukidhi matakwa ya leseni yanayolenga kuhakikisha mpira wa miguu unaendeshwa kwa weledi na kupiga vita upangaji matokeo katika maeneo matano ya wachezaji (sporting), viwanja (infrastructure), utawala (administrative and personnel), umiliki wa klabu (ownership) na fedha (financial), hazitapa leseni hivyo kutokuwa na sifa ya kushiriki ligi.

Klabu ambazo zitanyimwa leseni na kutoridhika na uamuzi huo, zitakuwa na fursa ya kukata rufani kwenye Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF. Kwa mujibu wa Ibara ya 5(3) ya Kanuni ya Leseni ya Klabu ya TFF, Kamati hiyo ndiyo inayosikiliza rufani zinazopinga uamuzi wa Kamati ya Leseni ya TFF.

Wajumbe wanaounda Kamati hiyo ni Wakili Alloyce Komba (Mwenyekit), Wakili Abdallah Gonzi (Makamu Mwenyekiti), Dk Francis Michael, Abdallah Mkumbura na Wakili Twaha Mtengela. Klabu zote zinahimizwa kuchukua fomu za maombi mapema ili kutoa muda wa kutosha kwa TFF kupitia maombi yao na kufanya uamuzi kwa wakati muafaka.

TFF YATOA KALENDA YA MWAKA, USAJILI KUANZA JUNI 15

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa kalenda ya msimu mpya wa mashindano na matukio ambako baada ya mapumziko ya wachazaji yanayoishia Juni 10, 2016.

Kalenda inaonesha kipindi kinachofuata sasa ni usajili unaotarajiwa kuanza Juni 15, 2016. Usajili huo unaanza na uhamisho wa wachezaji ambako utaanza Juni 15, 2016 hadi Julai 30, 2016.

Kwa mujibu wa Kalenda hiyo, timu ambazo hazishiriki Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2016/2017 zitaanza kutangaza wachezaji walioachwa kuanzia Juni 15, 2016 hadi Juni 30, mwaka huu.

Kwa upande wa timu zitakazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), watatumia kipindi cha Juni 15, 2016 hadi Juni 30, 2016 kutangaza usitishwaji mkataba wa wacheaji. Usajili wa utaanza Juni 15 hadi Agosti 6, kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Pingamizi itakuwa ni Agosti 7 hadi 14, 2016 kabla ya kuthibitisha usajili kwa hatua ya kwanza kati ya Agosti 15 na Agosti 19, 2016 wakati usajili hatua ya pili utaanza Agosti 17, 2016 hadi Septemba 7, 2016 na kitafuatiwa kipindi cha kipindi cha pingamzi hatua ya pili kuanzia Septemba 8 hadi Septemba 14, 2016.

Septemba 15 hadi Septemba 17, 2016 itakuwa ni kipindi cha kuthibitisha usajili hatua ya pili,

Ratiba hiyo inasema kwamba timu zinatakiwa kuandaliwa  kuanzi Juni 15 2016 hadi Julai 15, 2016 ambako kuanzia Julai 16, 2016 hadi Agosti 14 ni kipindi cha mechi za kirafiki za ndani na nje. Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itatoka kati ya Julai 16 hadi Agosti 14.


TFF YATANGAZA KOZI ZA UKOCHA

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Idara ya Ufundi, imetangaza kozi nne (4) za Leseni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinazotarajiwa kuanza Juni 20, 2016 katika mikoa ya Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam.

Kwa Mkoa wa Mwanza, TFF itaendesha kozi ya leseni Daraja C. kozi hiyo inatarajiwa kuanza Juni 20, 2016 hadi Julai 4, mwaka huu ambako baadhi ya washiriki 29 wamekwisha kujiandikisha ingawa bado kuna nafasi 11 ili kutimiza darasa la wanafuzni 40.

Sifa za watakaochukua kozi hiyo ni kuwa kuwa na cheti ngazi ya kati (intermediate) na umahiri (activeness).

Hii ni kozi ya CAF itakayoendeshwa na TFF na kwamba watu wenye ndoto za kuwa makocha wa mpira wa miguu wanaruhusiwa kuomba.

Kwa Jiji la Mwanza na mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, kozi hiyo inaratibiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya TFF, Vedastus Rufano anayepatikana kwa Namba ya simu 0753 772068 na Mwalimu atakuwa Wilfred Kidao ambaye ni Mkufunzi wa ukocha anayetambuliwa na CAF.

Mchango kwa ajili ya mkufunzi na uendeshaji Sh. 200,000 kwa kila mwanafunzi.

Kozi nyingine ni ya leseni Daraja B ambayo itafanyika kuanzia Julai 1, hadi Julai 16, mwaka huu mkoani Morogoro. Kozi hiyo ambayo mchango wake ni Sh. 300,000 kwa mwanafunzi tayari ina wanafunzi 35 na zimebaki nafasi tano tu na utaratibu wa kuijiunga unaratibiwa na Ofisi ya Idara ya Ufundi ya TFF iliyoko Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

Kozi nyingine ya leseni Daraja B inaratibiwa jijini Dar es Salaam ambayo kuanzia Julai 1, hadi Julai 16, mwaka huu ambako washiriki wa kozi hiyo ni ya TFF makocha ambao tayari walifanya kozi ya FIFA-IOC iliyofanyika Oktoba, 2014 hivyo kwa sasa wanatakiwa kuthibitisha kushiriki kabla ya Juni 15, 2016 katika ofisi ya Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi.

Nafasi pia zipo kwa washiriki wengine nje ya kundi la wale wa Oktoba, 2014 na kwamba sifa ni kuwa na Leseni Daraja C na awe amewahi kufanya kazi ya ukocha angalau kwa mwaka mmoja na zaidi. Mchango wa kozi hiyo ni Sh 300,000.

Kadhalika kozi nyingine ji ya Leseni Daraja  A ambayo itafanyika kuanzia Julai 17, 2016 hadi Julai 31, mwaka huu kwa hatua ya kwanza yaani Module 1 wakati Module 2 itafanyika Novemba, mwaka huu. Mchango wa kozi hiyo la Leseni Daraja A ni Sh 600,000 ambayo inalipwa kwa pamoja.

Wakufunzi wa kozi hiyo ya juu ni Makocha Salum Madadi na Sunday Kayuni, kabla ya CAF kumleta mtoa tathimini ya matokeo ya makocha hao kabla ya kutoa leseni ya daraja husika.

Washiriki wa kozi hiyo wanatarajiwa kuwa makocha wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwani msimu wa mwisho wa makocha wa Leseni Daraja B na C ni msimu wa 2016/2017.

Kuanzia msimu wa 2017/2018 hakuna kocha anayeruhusiwa kuongoza timu kwa kukaa kwenye benchi la ufundi kama hana sifa ya Daraja B na C. Msimu huu wa 2016/2017 ni nafasi ya mwisho kwa makocha wenye leseni madaraja ya chini kukaa au kuongoza timu za zinazoshiriki VPL.


IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Share on Google Plus

About trustedmishen

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment