Shirikisho la soka nchini T FF limetoa ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa mgongano uliyo jitokeza kati ya kamati ya utendaji ya shirikisho hilo na bodi ya ligi kuu ya soka ya Vodacom.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es salaam Rais wa shirikisho la soka nchini TFF
Jamali Malinzi amesema kuwa bodi ya ligi ya T F F ni
chombo cha TFF kama ilivyo kwa chombo kingine
Katika hatua nyingine Rais huyo
amesema kuwa bodi hiyo haina mamlaka ya kisheria ya aina yoyote ile Zaidi ya
TFF na washilika wake
ZAIDI UNAWEZA KUSIKILIZA HAPA
UFAFANUZI KUHUSU MAAMUZI YA KAMATI
YA UTENDAJI
Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti
kuhusu hali ya mgongano kati ya Kamati ya Utendaji ya TFF na Bodi ya ligi
Tanzania (Tanzania Premier league Board).
Shirikisho la mpira wa miguu
Tanzania linapenda kutoa ufafanuzi ufuatao:
1.Bodi ya ligi imeundwa kwa mujibu
wa Katiba ya TFF kifungu 40(11).Hivyo Bodi ya ligi ni zao la Mkutano Mkuu wa
TFF.
2.Katiba ya TFF imeipa mamlaka kamati ya utendaji ya TFF kutunga kanuni za
uendeshaji wa Bodi ya ligi,kanuni hizi ndiyo nguzo kuu ya uendeshaji wa
shughuli za Bodi ya ligi na ndizo zinaipa Bodi uhalali wake wa kuendesha
shughuli zake za kila siku.
3.Bodi ya ligi ni chombo cha TFF
kama vilivyo vyombo vingine vikiwemo kamati mbali mbali za TFF.Kisheria Bodi ya
ligi sio chombo huru (its not a legal entity) hivyo Bodi pamoja na mambo
mengine haina mamlaka ya kuingia mikataba ya aina yoyote ya kisheria .
4.Katiba ya TFF inatamka kuwa Bodi
ya ligi itaheshimu na kufuata maagizo ya TFF.Maagizo haya yanatolewa na
Sekretarieti ya TFF kwa niaba ya kamati
ya utendaji ya TFF.
5.Mwenye mamlaka ya kutengua maamuzi
ya kamati ya utendaji ya TFF ni Mkutano Mkuu wa TFF peke yake,hakuna chombo
kingine cha chini chenye mamlaka hayo.
6.Kanuni za mashindano zinaandaliwa
na kamati ya mashindano ya TFF na kupitishwa na kamati ya utendaji ya TFF.
Kikao cha kamati ya utendaji kilichopitisha
rasimu ya kanuni za ligi za mwaka 2014/15 kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa bodi
ya ligi,Makamu mwenyekiti wa Bodi ya ligi na pia Mwenyekiti wa kamati
ya mashindano ya TFF,hawa wote ni wajumbe wa Bodi ya ligi na walishiriki
kikamilifu katika kikao cha kamati ya utendaji kilichopitisha kanuni za ligi
2014/15 ukiwemo na utaratibu wa mgawanyo wa mapato ya milangoni na ya udhamini.
Katiba ya TFF inaagiza hivyo kuwa
Viongozi wakuu wa Bodi ya ligi watakuwa
pia ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF. Aidha mtendaji mkuu wa Bodi
ya ligi alikuwepo kwenye kikao hiki cha kamati ya utendaji kama mwajiriwa.
7. Uamuzi wa kuunda mfuko maalum wa
kuendeleza soka la vijana ni uamuzi uliopitishwa na kamati ya utendaji.
Lengo la kuanzishwa mfuko huu ni
kuwa na chombo maalum ambacho kitakuwa kinakusanya fedha toka vyanzo mbali
mbali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya soka la vijana nchini.Kwa sasa miradi
hii ni:
(a) Kuanzisha vituo vya kulea na
kuendeleza vipaji vya watoto kuanzia miaka 8-17
(sports centres) katika kila mkoa nchini mwetu.Mradi huu ni mkubwa
utahitaji nyenzo hasa walimu na vifaa.
(b) Kuandaa timu ya taifa umri chini
ya miaka 12 kwa ajili ya mashindano ya
Afrika umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Timu hii itaanza kuandaliwa mwaka huu
Desemba baada ya mashindano ya kitaifa umri chini ya miaka 12.
Hii timu itakusanywa na kuwekwa katika
shule moja ya bweni ambapo watalelewa na kuendelezwa vipaji vyao wakiwa pamoja
huku wanasoma.
Tanzania tumeomba kuwa wenyeji wa
fainali hizi.
(c) Kuandaa timu ya Taifa umri chini
ya miaka 14 kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika
umri chini ya miaka 17 mwaka 2017.
(d) Kuandaa timu ya Taifa umri chini
ya miaka 17 kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za
Afrika umri chini ya miaka 20 mwaka 2017.
(e) Kuandaa mashindano ya Taifa ya
mpira wa wanawake na ligi ya taifa ya mpira wa wanawake.
Miradi yote hii muhimu kwa maendeleo
ya mpira wa miguu Tanzania haina udhamini lakini ni lazima ifanyike ili
tujihakikishie tunainua mpira nchini mwetu.Mafanikio ya miradi hii sio tu
yatafaidisha na kuimarisha timu zetu za Taifa lakini pia yatakuwa chimbuko
madhubuti la wachezaji mahiri wa vilabu
vyetu vya mpira wa miguu.
Kimsingi tunatarajia kuwa vyanzo
vikuu vya mapato ya kutunisha mfuko wa maendeleo ya mpira Tanzania vitakuwa:
- Mapato yatokanayo na mechi za ligi
zetu madaraja yote
- Mapato yatokanayo na mechi za
kimataifa
- Wadhamini
- Serikali kuu kupitia bajeti za Wizara
zenye dhamana ya michezo,halmashauri na vyuo
- Wafadhili
- Shughuli mbali mbali za kutunisha
mfuko.
Kamati ya utendaji ya TFF ilimteua
Bwana Leodeger Tenga kuwa mwenyekiti wa kwanza wa mfuko huu na wajumbe wake ni
Bw Tarimba Abbas, Bw Ephraim Mafuru, Mzee Ayoub Chamshama Bw Frederick Mwakalebela na Mh Zarina Madabida.
Bw Henry Tandau na Bw Boniface Wambura ni waratibu wa mfuko huu. Imani ya TFF
ni kuwa wajumbe hawa kwa kutumia uzoefu wao katika uongozi wa jamii
watatusaidia kuhakikisha mfuko huu unaanza vyema shughuli zake.
Upande wa TFF tumefungua akaunti
maalum benki kwa ajili ya kuingiza fedha zote zinazokusanywa kama mchango wa
TFF kwenye mfuko huu zikiwemo asilimia 5 za makato ya fedha za udhamini na ZILE
zitokanazo na mfuko wa jichangie,TFF inatoa wito kwa wadau wote wa mpira wa
miguu Tanzania kuchangia mfuko huu ili utumike kunusuru mpira wetu. Fedha
zitakazokusanywa matumizi yake yatasimamiwa na kanuni za uendeshwaji wa mfuko
huu.
Hitimisho:
Kila mwanafamilia wa TFF anawajibika kuheshimu na kufuata maelekezo ya
Kanuni za mashindano ya ligi kuu kama zilivyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya
TFF .
Hivyo utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na
fedha za milangoni na za wadhamini kama ulivyoainishwa kwenye kanuni hizi uko
pale pale.
Ninaiagiza Bodi ya ligi kusimamia
utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya utendaji ya TFF mara moja. Mwenye
malalamiko kuhusu kanuni hizi ayalete
kwenye vyombo husika vya TFF kwa kufuata
Katiba,kanuni na taratibu za Shirikisho.
Sote tunajenga nyumba moja hakuna
haja ya kugombea fito.
0 comments:
Post a Comment