DIRISHA DOGO LA USAJILI LINATARAJIWA KUFUNGWA HII LEO PATA DONDOO KUHUSIANA NA KLABU ZILIKOFIKIA KUHUSU USAJILI ##

    Andrey coutinho hajavutia yanga sc baada ya mechi 11 akifunga mabao matatu
Wakati dirisha dogo la usajili linafungwa leo Saa 6:00 usiku,  klabu ya Yanga SC inafikiria kumuacha Mbrazil mmoja kati ya Andrey Coutinho na Emilson de Oliviera Rogue, ili imrejeshe Mganda Hamisi Kiiza, au isajili mchezaji mwingine.

Kiiza aliondoka kambini siku moja kabla ya mechi ya Nani Mtani  Jembe ambayo Yanga SC ilifungwa 2-0 na Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kufuatia taarifa kwamba yeye ndiye  atakayekatwa baada ya kusajiliwa Mliberia, Kpah Sean Sherman.

Lakini uongozi wa Yanga SC unasistiza bado haujamuacha mchezaji  huyo, ingawa taarifa zinasema alikwenda kujaribu kujiunga na  mahasimu, Simba SC ambako alikwama kwa sababu hakuwa na barua ya kutemwa na bado ana Mkataba na mwajiri wake wa sasa.

Kutemwa Kiiza ni pendekezo la kocha Mbrazil wa Yanga SC, Marcio Maximo, lakini uongozi wa klabu hiyo hadi sasa haujaafiki.

Kiiza aliondoka kambini kabla ya mechi ya nani mtani jembe.
Yanga SC hawajaridhishwa na uwezo wa Coutinho, aliyeichezea klabu  hiyo mechi 11 na kuifungia mabao matatu, lakini kikwazo ni Mkataba  wake mrefu ambao utawalazimu kumlipa fedha nyingi wakimuacha.

Wakala aliyemleta Mliberia, Sherman ambaye amewavutia wana Yanga  wengi baada ya kuichezea klabu hiyo kwa mara ya kwanza juzi,  amewahakikishia viongozi wa klabu hiyo anaweza kuwapatia mchezaji mwingine mzuri ndani ya Saa 12 na kukamilisha usajili wake wote.

Katika dirisha dogo, Yanga SC imesajili wachezaji watatu mbali na  Mbrazil Emerson na Mliberia Sherman, mwingine ni mzalendo mshambuliaji Dan Mrwanda.

Kwa upande wa Simba SC, jana imewasainisha mikataba wachezaji  wawili wa kimataifa wa Uganda, beki Juuko Murushid na mshambuliaji  Simon ‘Sam’ Sserunkuma, siku moja baada ya kuisaidia timu hiyo kushinda 2-0 dhidi ya Yanga SC.

Wawili hao wote walicheza juzi mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba SC  ikiwafunga mahasimu wao wa jadi, Yanga SC 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar  es Salaam mabao ya kipindi cha kwanza ya Awadh Juma na Elias Maguri.

Wawili hao wanachukua nafasi za Warundi kiungo Pierre Kwizera na  mshambuliaji Amisi Tambwe wanaotemwa na sasa wanaungana na Waganda  wenzao, beki Joseph Owino na washambuliaji Dan Sserunkuma na  Emmanuel Okwi kukamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni kwa  mujibu wa kanuni za Ligi Kuu.
Tambwe mfungaji bora wa ligi kuu bara msimu uliopita.

Tambwe aliyejiunga na Simba SC msimu uliopita pamoja na Mrundi  mwenzake, Gilbert Kaze aliyetemwa Desemba mwaka jana, anaondoka  Msimbazi baada ya kuichezea timu hiyo mechi 43 na kuifungia mabao  26.

Tambwe ndiye aliyeibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu  uliopita- baada ya kuivutia Simba SC akiichezea Vital’O ya Burundi  katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu Kombe la Kagame nchini Sudan mwaka jana na kuiwezesha kutwaa taji hilo naye  akiwa mfungaji bora.

Pierre Kwizera aliyesajiliwa kutoka Ivory Coast mwanzoni mwa  msimu, hadi anaondoka amecheza mechi 14 bila kufunga bao. 

Kwa upande wa Azam FC, imeongeza wachezaji watatu karika dirisha  dogo, ambao ni beki Serge Wawa Pascal raia wa Ivory Coast  aliyekuwa anacheza El Merreikh ya Sudan, winga wa Uganda Brian  Majwega aliyekuwa anacheza KCCA ya Kampala na kiungo mzalendo,  Amri Kiemba aliyetua kutoka Simba SC.

Wawa na Majwega wanaungana na pacha wa Ivory Coast, Kipre Tchetche  na Kipre Balou na Mrundi, Didier Kavumbangu kukamilisha idadi ya  wachezaji watano wa kigeni Azam FC, huku Leonel Saint- Preux wa  Haiti akitemwa.

Fahamu kuwa Azam FC inaridhika na uwezo wa Leonel kiuchezaji,  lakini nidhamu yake mbovu ambayo alikuwa amekwishaanza  kuwaambukiza wachezaji wengine waadilifu wa klabu hiyo, inafanywa  aachwe.

Habari kutoka ndani ya Azam FC zinasema kwamba Leonel alikuwa  mfano mbaya ndani ya kambi ya timu na alikwishaanza kuwaambukiza na wachezaji wengine tegemeo wa timu hiyo.
Tayari Azam FC imekwishaziba pengo la Mhaiti huyo kwa kumsajili  winga wa kimataifa wa Uganda, Brian Majwega.

Winga huyo wa KCCA ya Kampala, Uganda alisaini Mkataba wa miaka  miwili jana mjini Kampala, Uganda kujiunga na mabingwa hao wa  Tanzania Bara.

Majwega anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Azam FC katika  dirisha dogo baada ya beki Serge Wawa Pascal kutoka Ivory Coast,  aliyekuwa anacheza El Merreikh ya Sudan na Amri Kiemba aliyekuwa Simba SC, ambaye amesainiwa kwa mkopo hadi mwisho wa msimu.

Na anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kigeni, baada ya  Mrundi Didier Kavumbangu na Kipre Tchetche, Kipre Balou na Serge  Wawa wote kutoka Ivory Coast.

Majwega anatarajiwa kuanza mazoezi na kikosi cha Azam FC leo mjini  Kampala, chini ya makocha Mcameroon Joseph Marius Omog na Mganda  George ‘Best’ Nsimbe ambacho kipo kambini mjini humo tangu Ijumaa  hadi Desemba 22, mwaka huu.

Kwa upande  wa Vinara wa Ligi Kuu hadi sasa, Mtibwa Sugar wao wameimarisha kikosi chao kwa kumsajili mkongwe, Nahodha wa zamani  wa timu ya taifa ya  Tanzania, kiungo Henry Joseph Shindika aliyewika Simba SC kabla ya  kwenda Norway.

Zaidi ya hapo, Wakata Miwa hao wa Manungu wameendelea na utamaduni  wao wa kupandisha wachezaji chipukizi kutoka timu yao ya vijana.

Mbeya City imeimarisha safu yake ya ulinzi kwa kumsajili beki  mkongwe, Juma Said Nyosso, wakati Coastal Union imemsajili kiungo  Abdulhalim Humud ‘Gaucho’.

Lakini pia zipo taarifa kuwa Kiungo wa zamani wa Simba, Haruna  Moshi ‘Boban’, anatarajia kumalizana na Friends Rangers leo.
Boban anatarajiwa kujiunga na friend Rangers.

Friends Rangers ya daraja la kwanza imekuwa ikipambana kupanda ligi kuu.

Katibu Mkuu wa Friends Rangers, Herry Mzozo amesema wameshafanya  mazungumzo na Boban na wako katika hatua nzuri.

Boban amekaa msimu mzima bila ya kuichezea timu yoyote.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatarajiwa kutoa orodha kamili ya wachezaji waliongia katika klabu zote kwenye dirisha hili dogo baada ya Saa 6:00 usiku wa leo.
Share on Google Plus

About trustedmishen

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment