IDARA
ya Uhamiaji Tanzania imetoa vibali vya kufanyia kazi kwa wachezaji
wawili wa Simba SC, Mrundi Pierre Kwizera na Mkenya Paul Kiongera pamoja
na kocha wao, Patrick Phiri, lakini haijatoa kibali cha mshambuliaji
Mganda Emmanuel Okwi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema jioni hii kwamba wamefanikiwa kupata vibali vya wachezaji hao na kocha Phiri, lakini pamoja na kupeleka pia maombi kwa ajili ya kibali cha Okwi, hakijatoka.
Mapema jana, Idara ya Uhamiaji iliwazuia wanne hao kufanya kazi Simba SC hadi hapo watakapopatiwa vibali- lakini sasa wanaweza kuendelea na kazi, kasoro Okwi ambaye kibali chake kimekwama.
Simba SC inashuka dimbani Jumamosi hii kumenyana na Polisi Morogoro katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na maana yake iko hatarini kumkosa Okwi.
Okwi anaweza kukosekana katika wakati ambao Simba SC inamkosa mshambuliaji mwingine, Kiongera ambaye ni majeruhi anayetakiwa kuwa nje kwa wiki sita.
Simba SC pia itawakosa kipa Ivo Mapunda, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na winga Haroun Chanongo ambao wote ni majeruhi, lakini habari njema tu ni kwamba kiungo ‘mchapakazi’ Jonas Mkude yuko tayari kuanza kazi Jumamosi.
Mapunda ni majeruhi wa muda mrefu kama Kiongera, ambaye anatakiwa kuwa nje kwa wiki nane, wakati Issa na Chanongo wiki ijayo wanaweza kurudi kazini.
Haijulikani ‘zengwe’ la Okwi litachukua muda gani kumalizika kabla ya mchezaji huyo kurejea uwanjani.
0 comments:
Post a Comment